Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo anaanza ziara yake ya siku 4 Nchini India, Ziara ambayo Rais Samia kaambatana na Wafanyabiashara 100 kutoka Tanzania.
Wafanyabiashara hao wanatoka katika maeneo ambayo yanatafuta masoko zaidi au yanayohitaji mitaji zaidi na ushirikiano kutoka India ili yapige hatua.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba amesema serikali tayari imetenga eneo la ekari zaidi ya 1,000 nchini Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa viwanda kutoka India ili kukuza uwezo wa uzalishaji wa taifa hili na kuongeza ajira kwa Watanzania.
Eneo lingine ambalo limepewa umuhimu wa kipekee kwenye ziara hii ni suala la afya. India kwa sasa ni miongoni mwa mataifa yanayoongoza kwa uzalishaji wa dawa na matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye matibabu.
Rais Samia amewahi kuzungumza hadharani kwamba anaguswa sana na changamoto za kiafya zinazowakabili Watanzania na ziara hii inajibu mojawapo ya changamoto hizo.
Kwenye ziara hiyo ya kihistoria, Rais Samia anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo ya faragha na baadaye mkutano na waandishi wa habari na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi.
Pia atakutana na kuhudhuria dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na mwenyeji wake, Rais Droupadi Murmu, wa India mnamo Oktoba 9 mwaka huu.