Tanzania imetajwa kwa mafanikio katika Maonyesho ya Kimataifa ya Fruit Logistica 2025, Berlin, nchini Ujerumani, ambapo ilionyesha ubora wake katika tasnia ya horticulture, na kusababisha wafanyabiashara kusaini mikataba ya kuuza mazao ya horticulture yenye thamani ya mamilioni ya dola za kimarekani.
Taarifa kutoka kwa taasisi kilele ya kilimo cha horticulture nchini, Tanzania Horticultural Association (TAHA) iliyoshiriki Maonyesho hayo makubwa Duniani, inaonyesha kuwa wauzaji wa Tanzania wamesaini mikataba mingi ya kuuza mazao ya horticulture yenye thamani ya jumla ya Dola za Kimarekani zipatazo milioni $12.6, sawa na Shilingi bilioni 33.3/-
Kwa ujumla, kampuni moja ya kitanzania inayojishughulisha na kilimo cha horticulture imesaini mkataba kuiuzia kampuni kubwa ya Uingereza tani 500 za maharage mekundu ya sukari kwa kipindi cha miezi kumi yenye thamani ya dola za kimarekani milioni $4.4, sawa na shilingi bilioni 11.61/-.
Taarifa ya TAHA inasema kuwa kampuni hiyo hiyo pia imesaini mkataba wa kusambaza tani 125 za maharage ya kawaida kwa kampuni moja inayouza bidhaa za kilimo duniani, yenye thamani ya dola milioni $1.1, takribani bilioni 2.9/- kwa miezi kumi.
Zaidi ya hayo, kampuni moja kutoka Uingereza imethibitisha kuagiza kontena sita zenye futi 40 ya parachichi yanayozalishwa Tanzania kwa kila wiki, mkataba utakaoleta dola za kimarekani milioni $7.1 sawa na shilingi bilioni 18.74/- kwa miezi kumi.
Pia, Tanzania imevutia mashirika nane kutoka Uingereza yenye nia ya kununua viungo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na tangawizi, matunda aina ya passion, maharage, mimea ya mizizi yenye dawa, jambo linaloongeza fursa za kibiashara na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika soko la kimataifa.
Mtaalamu wa biashara wa TAHA nchini Uingereza, Bw. Maarten Boeye, amesema mazungumzo kuhusu kiasi cha bidhaa na bei za viungo yanaendelea na hivi karibuni mikataba itasainiwa.
Mauzo ya mazao hayo, yatatekelezwa kupitia Programu maalumu ya TAHA ya HEAP inayolenga kuboresha ufanisi wa mauzo ya mazao ya horticulture, ikiwa na lengo la kuuza mazao yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni mbili ifikapo 2030.
Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Hassan Idd Mwamweta, alishukuru juhudi za wafanyabiashara na TAHA, akisisitiza mafanikio haya ni matokeo ya ushirikiano wa kipekee kati ya sekta ya umma na binafsi.
“Tunawashukuru kwa dhati mshirika wetu wa kimaendeleo Trade Mark Afrika (TMA), Wizara ya Kilimo, COPRA, na TADB kwa msaada wao mwaka huu,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi.
Dkt Mkindi pia amewapongeza wafanyabiashara wote ambao wamekuwa wakishiriki katika maonyesho ya kimataifa na kutumia fursa nyingi zilizopo.
“Mafanikio haya ni ushahidi wa kujitolea kwetu pamoja na ushirikiano thabiti katika kukuza biashara ya mazao ya horticulture ya Tanzania na sekta ya kilimo kwa ujumla,” alimalizia Dkt. Mkindi.