Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI leo imewasilisha taarifa Bungeni Dodoma na kueleza kuwa Wafungwa na Mahabusu Tanzania wanapewa chakula cha aina moja tu ambacho ni ugali na maharagwe kila siku hali inayofanya wale walioathirika na virusi vya UKIMWI wanapokuwa wanatumia dawa za kufubaza virusi (ARVs) wazidi kudhoofika kiafya kwani dawa wanazotumia ni kali na zina nguvu sana.
Kamati hiyo imeishauri Serikali kuhakikisha lishe bora inatolewa kwa WAVIU waliopo magerezani ambapo takwimu zilizotolewa na Kamati hiyo zinaonesha kuwa magereza yote nchini yana jumla ya Wafungwa na Mahabusu 888 waliogundulika kuwa na VVU na wanatumia dawa.