KATIBU wa Halmashauri Kuu(NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi, Uenezi,Siasa na Mafunzo CPA Amoss Makala amewahakikishia Watanzania kwamba Chama hicho katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kimeweka wagombea safi ambao wako tayari kuleta kuleta maendeleo
CPA Makala ameyasema hayo leo Novemba 21,2024 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam ikiwa ni siku ya pili ya mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu huku akisisitiza uchaguzi huo ni muhimu sana kwani ni uchaguzi unaowezesha kupatikana viongozi wanaokwenda kuishi na wananchi.
“Naomba niwahakikishie Watanzania kwamba Chama Cha Mapinduzi kimeleta wagombea safi ambao wako tayari kuwatumikia katika kuleta maendeleo.Mchakato wa kupata wagombea wa CCM wamepatikana katika utaratibu wa demokrasia na ukweli wagombea hao wanayo dhamana ya kuhakikisha wanakwenda kushirikiana na madiwani,Wabunge na Rais katika kuleta maendeleo,”amesema CPA Makala.
Ameongeza kuwa CCM wagombea wake wameandaliwa na Wana sifa za kutosha za kuwatumikia wananchi wakati wagombea wa CHADEMA hata utaratibu wa kupata wagombea wake haueleweki kwani wanapena tu.”Utasikia wanapambana Kamanda chukua Mtaa huo..Kwa CCM wagombea wetu wanapatikana kwa utaratibu mzuri kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.”
Akizungumza zaidi mbele ya mamia ya wananchi wa Wilaya ya Kigamboni,CPA Makala amesema baada ya Chama hicho kuzindua kampeni zake rasmi jana nchini kote tayari wapinzani wameingia ubaridi maana wanaona tayari wameshandindwa huku akisisitiza CCM inatofautiana na vyama vingine vya siasa na kufafanua Chama hicho ndicho kina Ilani ya Uchaguzi Mkuu inayotekelezeka na wengine hawana.