Uganda imeruhusu wagonjwa wanane kuondoka hospitalini ambao wamepona kutokana na aina ya Sudan ya Ebola baada ya kupima vipimo vya ugonjwa huo mara mbili kwa tofauti ya saa 72.
Kufikia sasa, kifo kimoja tu ndio kimerekodiwa -muuguzi wa kiume wa miaka 32 pia watu 265 wanasalia kuwa kwenye karantini.
Wizara ya afya ilithibitisha kuwa wagonjwa hao wameondoka hospitalini na ikahimiza umma kutoendeleza unyanyapaa.
“Ninasihi familia zao na jamii ziwapokea na kutangamana nao kama kawaida,” Waziri wa Afya Dk. Jane Ruth Aceng Ocero alisema
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilisema wagonjwa kupona ni “hatua muhimu” katika kudhibiti mlipuko.
Wagonjwa walitibiwa mjini Kampala na eneo la Mbale, mashariki mwa Uganda.
Hakuna chanjo zilizoidhinishwa kwa aina ya Sudan ya Ebola.
Baada ya kutangaza mlipuko wa ugonjwa huo mwishoni mwa Januari, viongozi wa afya wa Uganda walichukua hatua haraka kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.
Mnamo mwezi Februari, Wizara ya Afya ilianzisha chanjo ya majaribio na kupanua utafiti katika chaguzi za matibabu.
Kwa msaada kutoka kwa washirika wa kimataifa, Uganda inaendelea kutoa huduma ya matibabu, kuimarisha juhudi za kuzuia, na kuongeza uhamasishaji wa jamii.