Wahudumu wa Afya katika Mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wameeleza kusikitishwa kwao na ukosefu wa Chanjo ya Mpox, hali inayoongeza kasi ya maambukizi ya Ugonjwa huo hatari.
Katika kituo cha tiba kilichoko katikati ya mlipuko huo, wahudumu wanakabiliana na wimbi kubwa la wagonjwa wapya kila siku, wakiwemo Watoto wachanga, huku vifaa vya msingi vikikosekana.
Mpox, Ugonjwa unaoambukiza kwa urahisi, umesababisha vifo vya watu 635 nchini DRC mwaka huu, Chanjo 200,000 zilizotolewa na Umoja ya Ulaya tayari ziliwasili Kinshasa wiki iliyopita, lakini hazijafikishwa Kivu Kusini, huku changamoto za usafirishaji na uhifadhi zikiwa kikwazo kikubwa.
Aidha Emmanuel Fikiri, muuguzi wa kituo hicho, amesema wanapata taarifa za Chanjo kupitia mitandao ya kijamii, lakini hadi sasa hawajapata msaada wowote wa moja kwa moja.
Changamoto za miundombinu duni, barabara mbovu, na uhaba wa vifaa vya kujikinga zimesababisha hali kuwa mbaya zaidi kwa wahudumu wa afya, na kwa kuwa Chanjo hizo zinahitaji kuhifadhiwa kwenye joto maalum, mpango wa kuzisafirisha unachukua muda mrefu, na huenda ukahitaji Helikopta ili kufika maeneo yenye mlipuko mkubwa kama Kamituga, Kavumu, na Lwiro.
Aidha Daktari Pacifique Karanzo, mmoja wa Wahudumu katika Kliniki hiyo, amesema ukosefu wa vifaa vya kinga na maji safi umesababisha Wagonjwa kushiriki vitanda na hata kulala sakafuni, hata hivyo, ameonyesha matumaini kidogo kutokana na ongezeko la ufahamu kuhusu Mpox miongoni mwa wakazi, jambo ambalo linaweza kusaidia kudhibiti mlipuko huo iwapo Chanjo na msaada zaidi utafikishwa haraka.