Wakala wa Vipimo katika utekelezaji wa majukumu yake imeendelea kutoa mchango katika kuchochea maendeleo ya sekta za kiuchumi na kijamii nchini, kuchochea uzalishaji wa bidhaa unaozingatia vipimo sahihi, kuendelea kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali.
Akizungumza katika kikao kilicho wakutanisha na wahariri pamoja na waandishi wa habari leo Septemba 11,2024 afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo(WMA), Alban Kihulla amesema atika utekelezaji wa majukumu yake wanasaidia katika kujenga uchumi wa kisasa, shirikishi na shindani, msingi mkuu wa kufanikisha haya ni kuwa na viwanda vinavyotumia ipasavyo vilivyohakikiwa na kukidhi matakwa ya kimataifa (Traceability to International Standards) ambavyo huongeza tija, ufanisi na usahihi wa vipimo vya bidhaa zinazozalishwa kwenye viwanda hivyo kuwa shindani katika soko la ndani na la nje matokeo yake ni kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na pato la Taifa.
Ameongeza kuwa ili kuleta ufanisi katika zoezi la ubora wa upimaji sahihi wa vipimo, elimu hutolewa juu ya umuhimu wa kufanya uhakiki wa Mizani inayotarajiwa kutumika katika kufanya ununuzi wa bidaa kufuatiwa na kaguzi za kustukiza wakati ununuzi wa bidhaa unaendelea ili kubaini watumiaji wa mizani wasiozingatia matumizi sahihi ya vipimo, taratibu na Sheria.
Afisa Alban Kihulla pia ametaja fursa kadhaa za uwekezaji unaoweza kufanywa na sekta binafsi katika tasnia ya vipimo nchini Tanzania na miongoni mwa fursa alizozitaja ni pamoja na sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa mizani mbalimbali na mita za maji, vifaa ambavyo amesema kwa sasa havizalishwi hapa nchini bali huagizwa kutoka nje ya nchi.
“Sisi jukumu letu linakuwa zaidi kwenye uhakiki wa vipimo,kwa sasa bado maeneo mengi yanahitaji vipimo vitumike, mathalani kwenye kilimo, mizani zinahitajika kwa wingi hivyo ni fursa kwa wenzetu wa sekta binafsi,” amesema Kihulla.
Akieleza zaidi kuhusu majukumu ya WMA, Kihulla amesema utekelezaji wake ni sehemu ya kusimamia Ilani ya Chama Tawala inayoitaka Wakala hiyo kuhakiki kwa ufanisi vipimo vyote vinavyotumika nchini ili kuzilinda pande zote mbili zinazohusika yaani walaji na wafanyabiashara .