Mamia ya Wakenya walihudhuria tamasha katika mji mkuu wa taifa hilo Nairobi siku ya Jumapili, wakiimba kauli mbiu na kucheza, kuadhimisha zaidi ya watu dazeni tatu waliouawa katika maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali.
Takriban watu 39 waliuawa katika maandamano hayo yaliyoanza Juni 18, huku waandamanaji wakishinikiza nyongeza ya ushuru iliyopangwa kufutwa na kujiuzulu kwa Rais William Ruto.
“Serikali inasikiliza sasa kwa sababu ya maandamano,kwa hivyo tuna furaha, lakini pia kuna huzuni nyingi kwa sababu watu wengi walikufa ili serikali isikilize,” mwanaharakati Boniface Mwangi, ambaye alikuwa akihudhuria tamasha hilo, alisema.
“Kwa hiyo sisi pia tunaomboleza, na tunawaambia familia za wale waliopoteza wapendwa wao, tuko pamoja nanyi, na tutaheshimu dhabihu yao.”