Upande wa Utetezi katika kesi ya kutekwa kwa Mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuendelea na kesi hiyo kwa kuwa mshtakiwa amekaa ndani muda mrefu.
Hayo yamebainishwa na Wakili wa utetezi, Mafulu Mbagwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya Wakili wa Serikali, Glory Mwenda kueleza upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Wakili Mbagwa amedai kuwa mshtakiwa huyo amekaa mahabusu kwa muda mrefu na washtakiwa wengine wako nje ya nchi na kama uwezekano wa kukamatwa haupo kesi hiyo iendelee.
“Tumekuwa tukisisitiza mshtakiwa amekaa ndani muda mrefu na kuna washtakiwa wako nje ya nchi na walieleza wametoa hati ya ukamataji tumeomba nakala lakini hatujapewa” amedai Wakili Mbagwa
Awali mahakama hiyo ilitoa hati ya kuwakamata washitakiwa watano ambao ni Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji na Phila Tshabalala ambaye ni raia wa Afrika Kusini.
Mmoja wa washtakiwa hao ambaye ameshafikishwa mahakamani hapo ni dereva wa taksi , mkazi wa Tegeta Mousa Twaleb.
Hakimu Shahidi ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 23,mwaka huu 2019.
Katika kesi hiyo inadaiwa Mei Mosi na Oktoba 10, 2018, katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Johannesburg Afrika Kusini, kwa makusudi washitakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu.
Pia inadaiwa Oktoba 11, 2018 maeneo Hoteli ya Colloseum wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Twaleb pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara MO kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.
Pia inadaiwa Julai 10, 2018 maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha ambazo ni Sh 8,000,000 wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.
MO alitekwa nyara Oktoba 11, 2018 alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo huo katika eneo la Gymkhana.
MUUAJI ATOKA GEREZANI KWA MSAMAHA WA MAGUFULI “NILIPIGANA DISCO, DAMU IKAVUJIA NDANI”