Wakimbizi 30 wamefariki kutokana na njaa na utapiamlo katika mkoa wa Gambela, kusini magharibi mwa Ethiopia.
Katika taarifa yake, Tume ya Haki ya Binadamu ya Ethiopia imesema, wakimbizi hao walifariki walipoondoka kwenye kambi zao kwenda kutafuta chakula.
Mkoa wa Gambela umepokea maelfu ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini, ambao walikimbia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyotokea mwaka 2013.
Katika miezi ya karibuni, mkoa huo pia umetoa hifadhi kwa maelfu ya wakimbizi wa Sudan wanaokimbia mapigano yaliyotokea katikati ya mwezi April mwaka huu.
Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa linakadiria kuwa, zaidi ya watu milioni 20 nchini Ethiopia walioathiriwa na ukame na mgogoro, wanahitaji msaada wa haraka wa chakula.