Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Iringa Bw. Reginaldo Msendekwa amefungua mafunzo kwa walimu wa sayansi na hisabati na kuwataka washiriki hao kwenda kuyatumia mafunzo hayo kuimarisha taaluma hususani matumizi ya TEHAMA shuleni.
Akifungua mafunzo hayo Januari, 25 2025 katika chuo cha Ualimu Kleruu kilichopo katika Manispaa ya Iringa amewaasa washiriki hao kwenda kuyatumia mafunzo watakayoyapata kuimarisha taaluma ili kuleta maendeleo pamoja na kutumia TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji kwa kuwa Dunia yetu inabadilika kila siku.
“Dunia inakwenda kwa kasi, masuala ya ufundishaji kwa kutumia mbinu za kizamani umepitwa na wakati kwa hiyo, tunahitaji walimu wetu wajiimarishe katika ufundishaji kwa kutumia TEHAMA, zana za kisasa za kisayansi” amesisitiza Msendekwa.
Aidha, amewataka washiriki hao kwenda kuboresha usalama wa mazingira ya shuleni ili ufundishaji na ujifunzaji ufanyike katika mazingira salama kwani bila mazingira salama wanafunzi hawataweza kufikia malengo yao na malengo ya Taifa
Kwa upande wake Richard Msigwa Mratibu wa Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) Ofisi ya Rais TAMISEMI amewataka washiriki hao kuwa wasikivu wakati wa mafunzo na kufafanua kuwa mradi huo umewezesha ujenzi wa madarasa janja ya kujifunzia, kununua vifaa vya maabara vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 10 na vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 18. Aidha, ameitaja mikoa inayoshiriki mafunzo hayo kuwa ni Dodoma, Iringa na Mbeya ikiwa na jumla ya washiriki 665 na Wathibiti Ubora (SQA) wapatao 17
Naye mwalimu Michael Mvalasau wa somo la hisabati kutoka shule ya sekodari Galigali iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ameishukuru Serikali kwa kutoa mafunzo ya walimu kazini kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwani yatawasaidia katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa msomo ya sayansi hususani matumizi ya TEHAMA shuleni pamoja na mabadiliko ya mitaala mipya ambayo imeanza kutumika mwaka huu kwa kidato cha kwanza.
Mafunzo hayo ya siku tano yanayotolewa kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari unaotekelezwa na SEQUIP kwa pamoja kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yana lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita kwa muda wa miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2026 na katika awamu hii ya pili ya mafunzo itafikisha idadi ya walimu 40,000 wa masomo ya sayansi na hisabati kote nchini.