Serikali ya Nigeria, hivi leo imewashtaki watu 10 kwa makosa ya uhaini na kuchochea jeshi kufanya uasi kufuatia maandamano ya kitaifa ya mwezi uliopita, ambapo maelfu ya raia walijitokeza kupinga kupanda kwa gharama ya maisha.
Wanaume 10 walifikishwa katika Mahakama Kuu ya Abuja ambapo walikana mashtaka dhidi yao, na ikiwa watapatikana na hatia watakabiliwa na adhabu ya kunyongwa.
Kwa mujibu wa hati ya waendesha mashtaka, wamedai kuwa raia hao walilenga kutatiza usalama wa nchi pamoja na kushirikiana kupanga njama za kuanzisha uasi.
Aidha mashtaka mengine ni pamoja na kulichochea jeshi kuasi, kuchoma moto majengo ya Serikali na kutatiza shughuli za kiuchumi.
Mahaka sasa inatarajiwa Septemba 11 kutoa uamuzi wa maombi ya dhamana ambayo yalipingwa na waendesha mastaka wa Serikali.
Tayari mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu yametoa wito kwa Serikali kuwaachi raia hao bila masharti, ambapo watu 13 waliuawa katika makabiliano na polisi.