Mahakama ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara katika kesi ya Uhujumu Uchumi Na.23/2017 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Kobero imewatia hatiani washtakiwa Mrisho Afrael na Iddi Maulid na kuwahukumu kwenda jela miaka 20 kwa kosa la kukutwa na Nyara za Serikali zenye thamani ya Tsh.34,500,000.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa wametenda kosa la kukutwa na Nyara za Serikali aina ya meno ya Tembo kinyume na kifungu cha sheria 86(1) na (2) cha Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori Na. 5/2009 inayosomeka pamoja na aya ya 14 ya 1 na kifungu 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Wakili wa Serikali Petro Ngassa aliieleza mahakama kuwa kosa hilo lilifanyika mnamo tarehe 3 Desemba, 2017 katika Kijiji cha Mayoka, Wilaya ya Babati, Mkoani Manyara ambapo watuhumiwa hao walikutwa na pembe mbili za ndovu bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Hifadhi ya Wanyamapori.
Katika kuthibitisha shtaka hilo upande wa mashtaka uliwakilishwa na mashahidi sita na vielelezo Saba na upande wa utetezi uliwakilishwa na mashahidi 4.