Wanafunzi wa Tanzania Washiriki Kambi ya Utafiti wa Vipaji vya Kidigitali ya Huawei Kusini mwa Jangwa la Sahara nchini China (leap digital study)
Shenzhen, ( Uchina) Huawei kwa mara nyingine tena imedhihirisha dhamira yake ya kuwawezesha vijana wenye vipaji katika nyanja za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kwa kuandaa Kambi ya Utafiti wa Vipaji vya Kidigitali ya Huawei kutoka katika nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara liliofanyika kuanzia Novemba 18 hadi Novemba 22, 2024 nchini China .
Mpango huo wa kidigitali umedhamiria kutoa maarifa ya Uongozi, na kutoa uwezekano wa fursa za kujiajiri ukilenga zaidi kukuza stadi za juu katika tasnia ya kidijitali na kukuza uvumbuzi miongoni mwa vipaji vya vijana kutoka kanda ya Afrika.
Kambi hiyo, iliyofanyika katika makao makuu ya kimataifa ya Huawei huko Shenzhen, ni sehemu ya dhamira pana ya Huawei ya kuendeleza wafanyakazi wenye ujuzi katika anga za kidijitali kote barani Afrika, ambapo pamoja wanafunzi wenye vipaji vya kipekee kutoka nchi 17 za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwa ni pamoja na Tanzania, Nigeria, Afrika Kusini. Mauritius, Kenya, na zaidi.
Kambi hiyo ya utafiti iligusa ajenda muhimu za kidigitali ikijumuisha kozi za ICT kuhusu teknolojia ya kisasa kama vile Akili Mnemba (AI), mawasiliano ya mtandao wa 5G, nguvu za kidijitali, teknolojia za masafa pamoja na kongamano la uongozi.
Tukio hilo la wiki moja lilifikia kilele kwa kuandaliwa shindano la Tech4Good, ambapo washiriki kutoka nchi tofauti waliandaa timu ili kuja na majawabu kupitia teknolojia yanayojibu changamoto za kijamii.
Tanzania iliwakilishwa na wanafunzi 10 bora kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT). Ambapo Huawei ilitoa ufadhili kamili kwa safari za ndege za kwenda na kurudi, malazi, na mafunzo kwa washiriki wote, ili kuhakikisha kwamba umakini wao unabaki kwenye kujifunza .
Kambi ya Utafiti wa Vipaji vya Kidijitali,ilizinduliwa na Huawei katika nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara mnamo mwaka 2022, ikiwa ni sehemu ya mpango wake mpana wa kukuza wafanyakazi wenye ujuzi katika anga za kidijitali kote barani Afrika.
Huawei inatazamiwa kuinua dhamira yake ya kuendeleza vipaji vya kidijitali katika Afrika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kutoa mafunzo kwa vijana 150,000 kupitia mpango wake wa kukuza ujuzi wa kidijitali katika miaka mitatu ijayo.
Mpango huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Huawei wa kuwekeza katika rasilimali za kimataifa zinazolenga kukidhi mahitaji mahususi ya vipaji vya kidijitali vya jumuiya za wenyeji.
Mpango huo umeundwa ili kuziba pengo la ujuzi wa kidijitali katika nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kutoa mafunzo na nyenzo za kina. Ikilenga katika kukuza uongozi wa kidijitali, kujenga wafanyakazi wenye ujuzi wa ICT, kuunda kundi la vijana wenye vipaji vya kidijitali, na kuimarisha ujuzi wa kidijitali miongoni mwa wananchi.
Kwa kufanya hivyo, Huawei inalenga kuleta athari kubwa kwenye uwezo wa kidijitali na matarajio ya siku za usoni za nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara.