Wanajeshi 25 wanaotuhumiwa kukimbia mapigano dhidi ya waasi wa M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) walihukumiwa kifo katika kesi ya siku moja Jumatano.
Mahakama ya kijeshi huko Kivu Kaskazini iliwapata na hatia ya wizi, kuwakimbia adui, na kukiuka amri, miongoni mwa mashtaka mengine.
Jeshi limekuwa likipambana na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka miwili, pamoja na kukabiliwa na ghasia kutoka kwa wanamgambo wengine.
Maafisa wa jeshi Jumanne waliwazuilia wanajeshi 27 na wake zao 4 raia, ambao walidaiwa kupokea bidhaa zilizoibwa kutoka kwa maduka katika kijiji cha jirani.
Walifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi ya Butembo siku iliyofuata.
Askari mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa wizi, huku wake wanne na askari mwingine waliachiwa huru.
Wote isipokuwa mmoja wa 25 walikanusha mashtaka. Wakili wao anasema atakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Mwezi Machi, DRC iliondoa kusitishwa kwa hukumu ya kifo, iliyokuwepo tangu mwaka 2003, ikitaja sababu ya usaliti na ujasusi katika migogoro ya mara kwa mara ya silaha.