Wanajeshi wapatao 23 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanakabiliwa na adhabu ya kifo au vifungo vya miaka 10 hadi 20 jela.
Ni baada ya kufikishwa mahakamani kwa mashitaka ya ubakaji, kuasi jeshi na uhalifu mwingine
Msemaji wa jeshi la Kongo Luteni Kanali MaK Hazukay amesema askari hao walifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi mjini Butembo katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Vikosi vya usalama kwa miaka mingi vimekuwa vikipambana na zaidi ya makundi 120 ya waasi katika eneo la mashariki mwa Kongo lenye utajiri wa madini.
Kongo iliondoa marufuku iliyodumu kwa miaka 20 ya adhabu ya kifo mwezi Machi, hatua iliyokosolewa na wanaharakati wa haki za binaadamu.
Mwezi Mei, askari wanane walihukumiwa adhabu ya kifo kwa kutoroka mapigano. Mwezi Julai, askari 25 walihukumiwa kwa makosa sawa na hayo. Haijabainika kama kuna yeyote kati yao aliyenyongwa.