Wanamgambo wasiopungua 50 wameuawa katika makabiliano makali baina ya maafisa usalama wa serikali ya Ethiopia na genge moja la wanamgambo katika eneo la Amhara, kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Taarifa ya Jeshi la Ulinzi la Ethiopia (ENDF) imesema, mapigano hayo yameshuhudiwa katika mji wa kihistoria wa Gondar, yapata kilomita 700 kaskazini mwa Addis Ababa, mji mkuu wa nchi hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, wanajeshi wa Ethiopia wamefanikiwa kuzima shambulizi la wanamgambo wa Harakati ya Kitaifa ya Amhara (FANO), ambapo 50 miongoni mwao wameangamizwa.
Hata hivyo taarifa iliyotolewa jana Jumatatu na genge hilo la Amhara National Movement imepuuzilia mbali taarifa ya jeshi la Ethiopia na kudai kuwa, kundi hilo limefanikiwa kuwatia nguvuni makumi ya wanajeshi wa serikali kuu.
Mapigano hayo makali yalizuka tangu Julai kati ya Jeshi la Ethiopia (ENDF) na wanamgambo wa FANO juu ya uamuzi wa serikali wa kuunganisha vikosi vya kikanda katika polisi wa shirikisho au jeshi.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Marta Hurtado, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa alisema, “Tunatiwa wasiwasi na kuvurugika hali ya haki za binadamu katika baadhi ya maeneo ya Ethiopia. Watu 183 wameuawa tokea Julai katika mapigano baina ya jeshi na wanamgambo wa kundi la FANO.”