Wananchi wa kata tano za Jimbo la Lupembe wilayani Njombe, wanatarajia kuondokana na adha ya kukodi usafiri kwa gharama kubwa pamoja na kupandisha wanawake wajawazito kwenye boda boda wanapofuata huduma kwenye hospitali kubwa mara baada ya serikali kuwaletea gari la kubebea wagonjwa.
Wakizungumza baada ya kukabidhiwa gari hilo katika kituo cha afya Mtwango na Mbunge wa Jimbo la Lupembe Edwin Swalle hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali.
Wananchi hao wamesema wanaishukuru serikali kwa kuhakikisha tatizo la kukosekana kwa gari la wagonjwa linaondoka ili kuwasaidia kuondokana na adha hiyo.
Mmoja wa wananchi hao akiwemo Sara Kaduma amesema wanayo furaha kuletewa gari la wagonjwa kwa ajili ya kuwawezesha usafiri pindi wanapopewa rufaa ya kufuata matibabu katika maeneo mengine.
“Ni kweli hospitali zipo, vituo vya afya vipo lakini pindi tunapotakiwa kwenda mbele zaidi labda mtu anatakiwa kujifungua anapandishwa kwenye boda boda mpaka anafika hospitali mtoto anakuwa amepata changamoto kwa hiyo vifo vingi vya mara kwa mara vya watoto vimetokea,” alisema Sara.
Awali Mbunge wa Jimbo la Lupembe Edwin Swalle alisema gari hilo linakwenda kuwaondolea wananchi adha kwa kiasi kikubwa na kueleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewapendelea kwa kutatua changamoto za afya katika jimbo hilo.
“Kuwa na gari la wagonjwa, kuwa na zahanati, vituo vya afya maana yake ni kwamba serikali na viongozi wenu wanapigania kuongeza umri wa kuishi wa watanzania. Tumpongeze sana mh Rais Samia kwa sababu tusipokuwa na afya bora, tusipokuwa na madawa kama hakuna magari ya kuwahisha watu hospitali ilikuwa uishi mwaka mmoja miwili unaondoka mapema,” alisema Swalle.
Swalle alisema wanawake wengi wajawazito wamepoteza maisha kutokana na kukosekana gari la wagonjwa kwa ajili ya kuwapeleka katika hospitali kubwa na kwamba walifia njiani wakiwa kwenye boda boda.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe,Valentino Hongoli alishukuru kwa kuletewa gari hilo na kueleza kuwa mbunge huyo amekuwa akifanya maendeleo bila ya kuangalia ukanda.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Christopher Sanga alisema walikuwa na kata tano ambazo zilikuwa zinakosa huduma ya gari la wagonjwa na kwamba uwepo wa gari hilo litasaidia wananchi kuondokana na adha hiyo.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mtwango, Beno Makero alisema walikuwa wanapata shida kwa sababu ya kukosekana kwa gari ya kubebea wagonjwa hivyo wakati mwengine walilazimika kukodi gari za watu binafsi ili kuwapeleka wagonjwa kwenye hospitali kubwa.