Wananchi wa Kijiji cha Kwedikwazu kilichopo wilayani Handeni mkoa wa Tanga wameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali zinazoendelea kufanyika ili kuleta maendeleo ya Kudumu kupitia Sekta ya Madini.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Kikundi cha Wanawake cha Mwanzo Mgumu, Bi Saumu Kisaka wakati akizungumza na timu ya Maafisa Habari wa Wizara ya Madini walipotembelea Mgodi wa Dolomite Mkoani humo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, Kisaka amesema, Kikundi chao ambacho kina wanachama 12 kinajishughulisha na biashara ya kokoto za mapambo, ujenzi na uuzaji wa mawe mbalimbali yakiwemo mawe ya ujenzi, biashara inayowasaidia kujipatia kipato na kuendesha maisha yao ya kila siku.
Pamoja na mambo mengine, akizungumzia uzoefu wake, Kisaka amesema biashara ya uuzaji madini ya Dolomite (mawe meupe) inamsaidia kuendesha maisha yake ikiwemo kusomesha watoto, kujenga nyumba ya kuishi na kukidhi mahitaji ya lazima ikiwemo gharama za matibabu, mavazi na chakula.
Katika hatua nyingine, Kisaka ameiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa masoko ya Madini hayo ya urembo na mashine ya usagaji wa mawe ambapo kwa sasa wanatumia nyundo za mkono kugonga mawe hayo ili kuongeza kipato kwa wananchi wanaoishi katika eneo la kijiji hicho na Tanzania kwa ujumla.