Ni Agosti 21, 2023 Wananchi takribani 200 wa Kata ya Mtitaa, Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma wadaiwa kuvamia mashamba ya zabibu na kuanza kuvuna zabibu bila ridhaa ya mwenye shamba.
Tukio hilo la kustaajabisha lilitokea baada ya wananchi hao kuwaswaga tembo waliokuwa wanapita katika njia yao kwa kuwapigia kelele na kuwafanyia fujo hali iliyosababisha tembo kuacha njia yao na kuvamia mashamba ya zabibu.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Mtendaji wa Kijiji cha Mtitaa, Bw. Hayaula Aloisi alisema “Tumezoea kuona tembo watatu wanne lakini safari hii kundi kubwa linalokadiriwa kuwa tembo 70 lilivamia katika kijiji chetu”.
Tembo hao walikuwa wanapita katika njia zao ambazo wamekuwa wakipita kila mwaka, kelele na fujo zilizofanywa na wananchi zilisababisha tembo kuacha njia yao na kuvamia shamba la zabibu huku wananchi nao wakitumia nafasi hiyo kuvuna zabibu na kufanya uharibifu mkubwa zaidi ya ule uliofanywa na Tembo.
Naye Afisa wa Uhifadhi Mkuu – Uhusiano kwa Umma TAWA Vick Kamata amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka kuhakikisha kwamba jukumu la kujikinga na wanyama wakali na waaribifu sio la mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori peke yake ila ni leru sisi Watanzania.