Serikali imeweka mikakati ya kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria na kitaaluma kikundi cha watu wachache ambao wamekuwa na tabia ya kuiba dawa za serikali kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima wakati wa kutoa salamu za Wizara kwa wakazi wa Wilaya ya Kahama kwenye ziara ya kikazi ya Rais Dk. John Magufuli.
Dk. Gwajima amesema kuwa kumekuwa na kikundi cha watu wachache kwenye eneo la kutumia ambalo limeshindwa kubadilika kutokana na watumishi hao kukosa uzalendo wa mali za nchi yao.
“Kikundi hicho tutakibaini na kuwachukulia hatua za kisheria kwani wamekuwa wakikwaza wanachi ambao wanaenda kupata huduma na kusababisha kukosa dawa kwa kudokoa dawa na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya serikali,” Dk. Gwajima
“Mbali na hatua za mahakamani watumishi wasio waadilifu watawajibika kwenye hatua za mwajiri na mabaraza yao ya kitaaluma,” Dk. Gwajima.