Serikali imesema kuwa ilibatilisha leseni za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yaliyokutwa na makosa mbalimbali yakiwemo ya kujihusisha na uhamishaji wa fedha nje ya nchi bila kuwa na leseni wala kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chumbuni, Mhe. Ussi Salum Pondeza, aliyetaka kufahamu sababu za maduka ya kubadilisha Fedha kuondolewa katika biashara na Wananchi wengi kupoteza ajira zao.
Mhe. Chande alisema kuwa mwaka 2016, Benki Kuu ya Tanzania ilifanya ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na kugundua miamala mbalimbali kwa baadhi ya maduka inafanyika kinyume na matakwa ya sheria na kanuni za usimamizi wa maduka ya fedha za kigeni na udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu.
“Mwaka 2018 na 2019, Benki Kuu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali ilifanya operesheni ya ukaguzi maalum kwenye maduka yote ya kubadilisha fedha za kigeni nchini na kubaini makosa mbalimbali yaliyosababisha Serikali kusitisha leseni kwa waliokiuka Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 36 (1)(b) na 2 (d) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2015 iliyorejewa mwaka 2019 ”, alisema Mhe. Chande.