Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesimama Bungeni leo na kutoa ufafanuzi na mwelekeo wa Serikali kuhusu changamoto ya nidhamu, malezi na adhabu zinazotolewa Shuleni, taarifa hii ameitoa ikiwa ni siku chache tangu kusambaa kwa taarifa zenye kuonesha matukio mengi dhidi ya Watoto kwenye Jamii na Shuleni.
Majaliwa amesema Serikali haitafumbia macho wala kukubaliana na aina ya adhabu kali Shuleni na tayari Serikali imechukua hatua za kinidhamu kwa Wahusuka huku akiwakumbusha Mamlaka za Elimu nchini kuhakikisha utoaji wa adhabu Shuleni unazingatia waraka namba 24 wa mwaka 2002 ambao umeainisha utaratibu wa utoaji wa adhabu.
Majaliwa ameesema baadhi utaratibu uliotolewa kwenye waraka huo ni pamoja na adhabu kuzingatia ukubwa wa kosa, jinsia na afya ya Mtoto na isizidi viboko vinne kwa wakati mmoja, pia Mwanafunzi wa kike anapaswa kupewa adhabu ya viboko mkononi na Mwalimu wa kike isipokuwa Shule hiyo kama haina Mwalimu wa kike, adhabu ya viboko itakapotolewa iorodheshwe katika kitabu kilichotengwa kwa kuonesha jina la Mwanafunzi, kosa alilotenda, idadi ya viboko na jina la Mwalimu aliyetoa adhabu.
Aidha Waziri Mkuu ametoa wito kwa wanaopata matukio haya kuwasilisha taarifa kwa Mamlaka husika na sio kuyarusha kupitia mitandao ya kijamii jambo ambalo linaleta taharuki na kwamba lengo sio kuficha taarifa bali ni kuzuia chuki na uhasama ndani ya Jamii na sio kwa Walimu tu bali kwenye nyanja zingine za utumishi kama Afya n.k.