Wafugaji na wafanyabiashara wote nchini wanaosafirisha mifugo kwenda nje ya nchi wametakiwa kuacha kununua mifugo katika Minada ya awali badala yake kwenda kununua kwenye ile ya Upili ili kuifanya sekta ya Mifugo kuwa kubwa na kuchangia pato la taifa.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 14, 2023 na Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia wizi wa Mifugo Nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Simon Pasua wakati akizungumza na Wafugaji pamoja na wafanyabiashara wa mifugo katika mnada wa Ndala uliopo wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
Kamanda Pasua amesema kuwa, kwenye minada ya awali havitolewi vibali vya kusafirisha mifugo kwenda nje ya nchi, hivyo waende kwenye minada ya Upili ama ya mpakani ambayo ni mikubwa na maafisa kutoka Wizara ya Mifugo wanapatikana huko kwa ajili ya kuvitoa.
Aidha amesema Jeshi hilo linaendelea kutoa elimu katika minada yote nchini na kubainisha kuwa kupitia elimu hizo pamoja na mambo mengine wafugaji wanaelimishwa namna bora ya kufanya biashara bila kununua mifugo ya wizi ama ile yenye migogoro.
ACP Pasua amebainisha kuwa kwa wale ambao watabainika kusafirisha mifugo hiyo bila kufuata utaratibu kwa kukwepa kulipa ushuru ama kutokuwa na vibali, Jeshi hilo litachukua hatua za kisheria dhidi yao ikiwemo kukamata mifugo hiyo na kuwafikisha wahusika Mahakamani.
Kwa upande wake bwana Methew Kabundala kwa niaba ya Wafugaji amebainisha kuwa tatizo linalowakabili katika mnada huo ni mifugo kuwa mingi zaidi ya miundombinu ya mazizi hali inayopelekea biashara kufanyika nje, Hivyo akaiomba Serikali kuboresha mnada huo ili uweze kukidhi mahitaji.