Polisi nchini Kenya wanachunguza, kuuawa kwa wanaume wanne, wanaodaiwa kuvuka mpaka na kuingia kwenye shamba la mananasi la Del Monte, katika Kaunti ya Murang’a Kilomita 50 kutoka jiji kuu Nairobi
Wanaume hao wanne wamegundulika kuuawa baada ya kuripotiwa kutoweka wiki iliyopita, na miili yao kupatikana ndani ya mto, Jumapili iliyopita.
Kamishena wa Kaunti ya Murang’a Patrick Mukuria, amesema uchunguzi umeanza kubaini namna wanaume hao walivyouawa, lakini hakueleza taarifa za kina.
Kampuni ya Del Monte, kutoka Marekani inayomiliki mashamba ya matunda na mboga mboga nchini Kenya, imesema mkanda wao wa video umewaonesha wanaume hao wakikimbilia mtoni walipokuwa wanafuatwa na walinzi baada ya kuiba mananasi.
Aidha, uongozi wa kampuni hiyo imesema, inashirikiana na mamlaka ya usalama nchini Kenya, kuchunguza namna wanaume hao walivyouawa.