Kufuatia maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani yanayofanyika kila tarehe 08/03, wanawake wa kata ya Kideleko katika halmashauri ya mji wa Handeni wametumia nafasi hiyo kupanda miti na kufanya usafi katika bwawa la maji la Kwamaizi katika kata hiyo. Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Handeni Trunk Main, Bw. Yohana Mgaza alisema:
“Toka kuzinduliwa kwake mwaka jana, bwawa la Kwamaizi limekua ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa kata ya Kideleko hasa wakinamama ambao wao ndio wana jukumu la kutafuta maji kila siku, hivyo tukaona ni vyema kutumia siku hii kulishafisha na kupanda miti rafiki kuzunguka bwawa hili ili liweze kudumu katika muda uliokusudiwa”
Bwawa la Kwamaizi katika halmashauri ya Handeni lilikamilishwa chini ya Ufadhili wa Kampuni ya bia ya Serengeti na kusimamiwa na shirika lisilo la kiserikali la WaterAid ambapo tangu kukamilika kwake mwaka jana linahudumia takribani wananchi 1944. Akizungumzia nafasi ya kinamama katika usimamizi wa miradi ya maji na usafi wa mazingira, Mwakilishi wa mkurugenzi wa shirika la WaterAid Tanzania, Bi. Neema Kimaro alisema:
“Licha ya mradi huu kulenga huduma ya maji safi kwa wananchi, pia, kuliundwa kikundi maalum cha wakina mama 24 waliosajiliwa kwa kazi maalum ya kuwezesha jitihada za kusimamia maswala yote ya uhifadhi wa Mazingira na ulinzi wa miundombinu ya maji ikiwemo usafi katika bwawa. Kikundi hiki kitafanya majukumu yake kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira – HTM wakiratibiwa na kusimamiwa na Halmashauri ya Mji wa Handeni.”
Mara baada ya kumaliza zoezi la upandaji miti katika bwawa hilo, mnufaika na mwenyekiti wa kikundi cha kinamama wanaosimamia mradi huo alimalizia kwa kusema:
“Lengo la hiki kikundi chetu cha kinamama ni kusimamia mauzo ya maji katika hili bwawa ila pia kusimamia matunzo na usafi wa mazingira kwa ujumla katika eneo linalozunguka bwawa.
Nchini Tanzania kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani ni “Wekeza katika wanawake: Kuharakisha maendeleo”.