Mbunge wa jimbo la Ulanga mkoani Morogoro Mhe Salim Alaudin Hasham Almas amewaomba wakala wa huduma za misitu Tanzania (Tfs) kuachia pikipiki za vijana wa bodaboda walizozishikilia kwa kosa la ubebaji mkaa bila kibali kwani vijana hao hawakupewa elimu ya kutosha kuhusu namna bora ya kufanya biashara hiyo.
Akiongea mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Dkt Julius Ningu mbunge huyo amesema chanzo cha vijana hao kutenda kosa hilo limetokana na wakala hao kutokuwa karibu na wafanyabiashara wa mazao ya misitu hivyo kupelekea watu kuvunja sheria pasipo kujua kwa kukosa elimu stahiki ya namna bora ya kufanya biashara hiyo.
Pia Mbunge Salim Almas amewataka vijana wa bodaboda kuacha kuvunja sheria kwa makusudi baada ya wao kupewa elimu kwa kutegemea viongozi wao watawatetea kwani kwa kufanya hivyo itarudisha nyuma maendeleo ya wilaya yao pamoja na nchi kwa ujumla.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Dkt Julius Ningu amemuagiza meneja wa wakala wa Huduma za misitu wilaya hiyo Ndg. John Willium Kalabaka kuachia pikipiki zote zikizoshikiliwa kwaajili ya kosa la kubeba mkaa na kisha aandae utaratibu maalum ambao utamfanya mfanyabiashara aelewe namna bora ya kufanya biashara hiyo kwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa ili kulinda misitu hiyo.
Hata hivyo Mkuu wa wilaya Dkt.Ningu pia ametoa siku 10 kwa Uongozi huo wa wakala wa huduma za misitu kuangalia namna bora ya kuwawezesha vijana hao kufanya biashara zao bila changamoto yoyote ili kuondoa migongano ya mara kwa mara kwani ni haki ya kila Mtanzania kufanya biashara halali ndani ya nchi yake bila kubughuziwa kwa kufuata sheria.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ulanga Ndg. Edson william Solly amewaomba wataalamu wa wilaya hiyo kuwasaidia wananchi katika kutatua changamoto zao na sio kuwakandamiza kwani kwa kufanya hivyo tunawarudishe nyuma kimaendeleo.
Zaidi ya pikipiki 30 zilishikiliwa kwa kosa hilo la kubeba mkaa bila kibali maalum na tayari pikipiki hizo zinafanyiwa utaratibu wa kurejeshwa kwa wamiliki pamoja na kupatiwa elimu ili kuepusha uvunjifu wa sheria kwa wakati mwengine.