Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Rufani Mhe. Jacobs Mwambegele, amefungua mkutano wa siku moja na wadau wa uchaguzi mkoani Tanga leo, Februari 1, 2025. Mkutano huu ni sehemu ya maandalizi ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura kwa mikoa ya Pwani na Tanga, ambalo litafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 19 Februari, 2025.
Zoezi hili litahusisha Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halmashauri za Miji ya Handeni na Korogwe, pamoja na Halmashauri za Wilaya ya Kilindi, Lushoto, na Muheza. Katika kipindi hiki cha siku saba, inatarajiwa kuwa wapiga kura wapya 431,016 wataandikishwa, na hivyo kufanya jumla ya wapiga kura katika mikoa hiyo kufikia 2,727,318 baada ya zoezi kukamilika.
Mhe. Mwambegele amesisitiza umuhimu wa wadau wa uchaguzi kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa. Ameeleza kuwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ni hatua muhimu katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.
Aidha, Tume imejipanga vizuri kwa ajili ya zoezi hili kwa kununua vifaa vipya vya BVR (Biometric Voter Registration) 6,000 ambavyo ni rahisi kubeba na vitasaidia kurahisisha zoezi la uboreshaji, hasa katika maeneo ya vijijini ambapo watendaji hulazimika kubeba vifaa kwa umbali mrefu.
Pia Tume inatoa wito kwa wananchi wote wenye sifa za kupiga kura katika mikoa ya Pwani na Tanga kujitokeza kwa wingi katika vituo vya uandikishaji ili kujiandikisha na kuboresha taarifa zao. Pia, inawahimiza wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa dini, asasi za kiraia, na vyama vya siasa, kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa zoezi hili.
Aidha wadau walioshiriki ambao ni vyama vya siasa,asasi za kiraia,wawakilishi wa wanawake,viongozi wa dini ,wawakilishi wa vijana na wazee wa kimila walishiriki katika mkutano wa Tume na wadau wa Uchaguzi na kutoa Maoni yao.
Kwa taarifa zaidi na ratiba ya uboreshaji kwa mikoa mingine, wananchi wanashauriwa kutembelea tovuti rasmi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi: