Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) limesema maonesho ya wazalishaji Tanzania 2024 yanatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 500 kutoka ndani na nje ya nchi huku zaidi ya nchi 21 zikitajwa kushiriki.
Aidha, limesema faida ya maonesho hayo kwa nchi ni kuhamasisha maendeleo ya viwanda kwa kuona bidhaa mbalimbali kutoka kwa wengine sambamba na kubadilishana ubunifu na kujengeana uzoefu.
Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la viwanda Tanzania (CTI), Leodgar Tenga katika mkutano na waandishi wa habari uliolenga kuujulisha umma juu ya maandalizi ya maonesho ya wazalishaji Tanzania maarufu kama TIMEXPO 2024 yatakayoanza tarehe 26 Septemba hadi oktoba 2.
Aidha, Tenga amesema pia kutakuwa msisitizo wa kuongeza ubora wa bidhaa tunazotengeza nchini ili kufanikisha ushindani pamoja na uwepo wa semina zitakazo saidia kuwaongezea uwezo washiriki ili kuepuka na na bidhaa zisizo na ubora hali ambayo inapelekea kutoweza kushindana.
Pia, amewataka watanzania kujitokeza kutazama bidhaa mpya sambamba na kuona teknolojia mpya katika sekta nzima ya viwanda kupitia maonesho hayo.
Kwa Upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Biashara- TANTRADE, Tito Nombo amesema maonesho hayo hayana kiingilio na TANTRADE imejiandaa vya kutosha na usajili wa washiriki unaendelea pamoja na kuandaa kumbi za matukio kwaajili ya kuhudumia maonesho hayo.