Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ndg Karia Rajabu Magaro Septemba 26,2024 ametoa maelekezo kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 27,2024.
Katika Kikao hicho kilichowakutanisha Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji, Wawakilishi wa vyama vya siasa, Asasi za Kiraia, Wazee maarufu na Viongozi wa dini, Magaro amewasihi wajumbe hao kila mmoja kwa nafasi yake kufikisha taarifa kwa watu walio chini yake.
Kwa Mujubu wa kanuni ya 9 ya Uchaguzi kanuni ya Uchaguzi Serikali za Mitaa 2024 Msimamizi wa Uchaguzi amepewa Mamlaka ya kutoa maelekezo kuhusu Uchaguzi.
Aidha msimamizi wa Uchaguzi amesema maelekezo kuhusu Uchaguzi yanatolewa siku sitini na mbili (62) kabla ya siku ya Uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha kuwa taratibu zote zinafuatwa na kwamba wapiga kura pamoja na wagombea wanapata taarifa zote zinazohitajika kwa wakati.
Pamoja na hayo, Magaro amewaeleza wajumbe hao kuwa kwa Mujibu wa kanuni ya 17 gazeti la Serikali namba 571,572,573 na 574 kanuni ya 16 gazeti la Serikali namba 572 wakazi wenye umri wa miaka 21 au zaidi wanaotaka kugombea nafasi za Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kitongoji, wajumbe wa Halmashauri ya kijiji na wajumbe wa viti Maalum wanahimizwa kuchukua fomu ya kugombea katika ofisi ya Msimamizi msaidizi wa Uchaguzi.
Vile vile Magaro amewasihi wajumbe hao kuzingatia kanuni zote za Uchaguzi kama walivyoelekezwa ili zoezi la Uchaguzi liweze kwenda kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda wa kuchukua na kurejesha fomu ifikapo Novemba 1 hadi 7.
“Tuna amini kila mmoja atazingatia kanuni ili kila mmoja apate haki ya ushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27,2024” amesisitiza Ndg Magaro ambaye ni msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Halmashauri.
Pamoja na hayo Magaro ametoa wito kwa Wananchi wote wenye sifa zinazohitajika kujitokeza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uchaguzi”
” Tunawasisitiza Wananchi kujitokeza kushiriki kwani Serikali inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan imetenga fedha kuandaa vifaa kwa ajili ya zoezi hili muhimu la Uchaguzi” amesema Magaro.
Akihitimisha kutoa maelekezo kuelekea Uchaguzi wa Serikali za mitaa, ndg Magaro amewasihi wajumbe hao kuwahamasisha watu wenye mahitaji maalum kushiriki vema machakato wa Uchaguzi ili kuendelea kukuza demokrasia na kuhakikisha upatikanaji wa Viongozi bora kwa Maendeleo ya Taifa letu.