Watanzania wanatarajiwa kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii zitakazopatikana kuelekea mashindano ya CHAN 2025 na AFCON 2027.
Hayo yamebainishwa leo Januari 15, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Michezo kuelekea CHAN 2025 na AFCON 2027 jijini Dar es Salaam.
“Nchi yetu imepata heshima kubwa kimataifa na hii haiji kwa bahati mbaya imesababishwa na ukuaji wa demokrasia iliyojengwa na Rais Samia kwenye mataifa mbalimbali duniani, ” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amewapongeza wadau wa michezo waliotoa mawazo ya kuanzishwa kwa kongamano hilo ili kutangaziana fursa zitakazotokea wakati wa mashindano hayo.
Ameeleza kuwa, mashindano yatawakutanisha wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali na kuna wajibu wa kufanya maandalizi kwa ufanisi mkubwa ili kunufaika na mashindano kupitia fursa mbalimbali za usafirishaji, malazi na burudani.