JESHI la Polisi mkoani Iringa linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Christina Kibiki.
Kada huyo aliuawa usiku wa kuamkia Novemba 13, mwaka huu, nyumbani kwake baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi, alisema baada ya kutokea kwa kifo hicho waliendesha operesheni na kuwakamata watu mbalimbali ambao waliwahoji.
Kamanda Bukumbi alisema wanaendelea na msako wa kuwakamata watuhumiwa wengine na kwamba kuna baadhi watawakamata muda wowote kuanzia sasa upelelezi utakapokamilika na kufikishwa mahakamani.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wa kuwafichua wahalifu kwa kuwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi na wananchi utasaidia kupunguza uhalifu.
Katika tukio lingine, Kamanda Bukumbi alisema Jeshi la Polisi mkoani humo linamsaka askari polisi Rogers mwenye namba F.4987 wa Kituo cha Polisi Ipogolo, pamoja na askari wa Jeshi la Akiba, Thomas Mkembela kwa tuhuma za kumuua Nashon Kiyeyeu (23), mkazi wa Nyamhanga, Kata ya Kitwiru, Manispaa ya Iringa.
Kamanda Bukumbi alisema mauaji hayo yalitokea Desemba 14, mwaka huu, na Sajenti Rogers kwa kushirikiana na mgambo walimkamata mtuhumiwa huyo kwa kuiba simu na kumpiga hadi kupoteza fahamu.