Vijana wameathiriwa zaidi na milipuko ya Mpox barani Afrika, huku watoto chini ya miaka mitano wakichangia karibu theluthi moja ya visa hivyo nchini Burundi, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto lilisema Ijumaa.
Burundi ni nchi ya pili barani humo kukumbwa na matatizo baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
“Watoto nchini Burundi wanabeba mzigo mkubwa wa mlipuko wa mpox, na viwango vya kutisha vya maambukizo na athari mbaya za kiafya,” Paul Ngwakum, Mshauri wa Afya wa UNICEF Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika alisema.
Ngwakum alisema theluthi mbili ya kesi nchini Burundi zilihusu watu wenye umri wa miaka 19 na chini.
“Kinachotia wasi wasi ni kuongezeka kwa ugonjwa wa mpox miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, ikiwa ni asilimia 30 ya kesi zilizoripotiwa,” aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva, akizungumza kupitia kiunga cha video kutoka Bujumbura.
Mpoksi, ambayo awali ilijulikana kama monkeypox, husababishwa na virusi vinavyopitishwa kwa wanadamu na wanyama walioambukizwa lakini pia inaweza kupitishwa kutoka kwa binadamu hadi kwa binadamu kwa kuwasiliana karibu kimwili.
Husababisha homa, maumivu ya misuli na vidonda vikubwa vya ngozi kama majipu, na wakati mwingine inaweza kuwa mbaya.