Takriban watu 20 wamepoteza maisha katika tukio la mkanyagano lililotokea katika zoezi la ugawaji chakula katika Jimbo la Anambra, kusini mashariki mwa Nigeria.
Mkanyagano huo wa watu umetokea katika mji wa Okija katika eneo la Ihiala baada ya mfanyabishara mmoja mtajika kujitolea kuwagawia watu chakula kabla ya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi.
Mkanyagano huo uliouwa watu wasiopungua 20 umetokea katika makazi ya Ernest Obiejesi, mfanyababiashara na mfadhili mashuhuri wa nchini Nigeria. Aghalabu ya waliopoteza maisha ni wanawake.
Baadhi ya majeruhi walikimbizwa katika hospitali za karibu kwa matibabu mbali na idadi ya raia waliothibitishwa kuaga dunia katika tukio hilo.
Charles Aburime msemaji wa Gavana wa jimbo la Anambra amesema serikali ya jimbo hilo imepata taarifa kuhusu hali ya mambo na itatoa taarifa baada ya uchunguzi kukamilika.
Mkanyagano huu umetokea katika jimbo Anambra siku kadhaa baada ya watoto 35 kupoteza maisha katika mkanyagano mwingine katika tamasha la wanafunzi huko Ibadan, kusini magharibi mwa Nigeria.