Kulingana na ripoti Umoja wa Mataifa unasema kuwa takriban watu 700 wameuawa katika mapigano makali huko Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, tangu Jumapili.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric anasema watu 2,800 walijeruhiwa wakati kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda lilipochukua mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.
Wapiganaji hao sasa wanasemekana kuelekea kusini kuelekea mji wa Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini.
Migogoro mashariki mwa Kongo ilianza miaka ya 1990, lakini imeongezeka sana katika wiki za hivi karibuni.
Vuguvugu la M23 linaloundwa hasa na Watutsi, linasema kuwa linapigania haki za walio wachache, huku serikali ya Congo ikisema kuwa vuguvugu hilo linaungwa mkono na Rwanda, kutaka kudhibiti eneo hilo la mashariki lenye utajiri wa madini.