Ndege za Israel mapema Jumatatu zilianzisha mashambulizi makali kaskazini-magharibi mwa mji wa Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza na kuua na kujeruhi makumi ya watu.
Vyanzo vya habari vya ndani viliripoti kwa shirika la habari la Palestina Wafa kwamba ndege za kivita za Israel zilirusha makumi ya makombora katika mji wa makazi wa Hamad, kaskazini-magharibi mwa Khan Yunis na kuua makumi ya raia wengi wao wakiwa watoto na wanawake na kuwajeruhi wengine. Vikosi vya Israel pia vilivamia mji wa Bani Suhaila, mashariki mwa Khan Yunis.
Vyanzo hivyo pia viliiambia Wafa: “Jeshi la uvamizi lilifyatua risasi za moto moja kwa moja kwenye Hospitali ya Indonesia, ambayo ilikuwa imejaa watu waliojeruhiwa. Raia kadhaa walijeruhiwa, akiwemo daktari.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, shambulio la bomu la Israel lilisababisha “kukatika kwa umeme katika hospitali hiyo baada ya jenereta zake kuacha kufanya kazi.”
Shirika hilo limebaini kuwa eneo la karibu na hospitali ya Al-Awda kaskazini mwa Ukanda wa Gaza pia lililipuliwa, na nyumba moja katika kitongoji cha Al-Daraj katika mji wa Gaza ilipigwa makombora kadhaa, na kujeruhi idadi ya raia ambao walipelekwa katika Hospitali ya Indonesia. .
Raia kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa kutokana na shambulizi la kivita la Israel lililolenga eneo la Asqoula katika kitongoji cha Al-Zaytoun, kusini mwa Mji wa Gaza.
Mlipuko mwingine wa bomu katika kitongoji cha Al-Sabra uliwaacha makumi ya raia wakiwa wamenasa chini ya vifusi.