Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mara Januari 15, 2021 mbele ya Jaji Mustapha Siyani katika Kesi ya Jinai Na. 56 ya Mwaka 2018 Jamhuri dhidi ya Juma Mugaya na wenzake 8, katika Kesi ya mauaji ya watu 17 maarufu kama kesi ya Mugaranjabo, imewatia hatiani washtakiwa sita na kuwapa adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa makosa yote 17 ya kuua watu wa familia moja ili kulipiza kisasi kutokana na ndugu yao Fred Mugaya kuuawa na wananchi kwa tuhuma za wizi wa mifugo.
Ilielezwa Mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Februari 16, 2010 katika eneo la Mugaranjambo lililopo Musoma Mkoa wa Mara ili kulipiza kisasi kwa kuwaua watu 17 wa familia moja kama sehemu ya kulipiza kisasi kutokana na ndugu yao marehemu Fredy Mugaya kuuawa na wananchi wa Mgaranjambo mwaka 2005 kwa tuhuma za wizi wa mifugo baada ya mzee wa familia hiyo marehemu Kawawa Kinguye kupiga yowe wakati wizi wa mifugo unafanyika nyumbani kwake hivyo baada ya tukio hilo washitakiwa walipanga kulipa kisasi na siku ya tukio walitekeleza kwa kuwakata kwa mapanga na kuwauwa watu kumi na Saba(17) wa familia moja huku wengine watatu wakiwaacha na vilema vya kudumu.
Awali kesi hi ilikuwa na washtakiwa kumi na sita lakini wengine walifariki vifo vya kawaida wakiwa magereza kabla ya a kesi kusikilizwa.
Akitoa hukumu Jaji wa Mahakama Kuu Mustapha Siyani aliwatia hatiani washitakiwa sita na kutoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa na kuwaachia huru washtakiwa watatu.
Waliotiwa hatiani ni Juma Mugaya, Aloyce Nyabasi, Nyakaranga Wambura Biraso, Nyakaranga Masemere Mugaya, Sadock Alphonce Ikaka na Kumbasa Buruai Bwire na walioachiwa huru ni Marwa Maua Mugaya, Ngoso Mgendi Ngoso na Sura Bukaba Sura.
Kesi hii iliendeshwa na Mawakili wa Serikali Renatus Mkude,Valence Mayenga, Robert Kidando, Ignatus Mwinuka na Yese Temba ambapo upande wa utetezi uliwakilishwa na mawakili tisa.