Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deogratius Ndejembi amemtaka Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga kufanya usanifu wa barabara ya Mwembesupu – Kwa Pepeteka- Bangulo yenye urefu wa kilomita moja katika Kata ya Pugu Stesheni ili kuanisha mahitaji halisi ya ujenzi na kuiwezesha Serikali kuiingiza kwenye mpango wa matengenezo kwa kiwango cha lami ambao utawawezesha wananchi wa Pugu kupata huduma za kijamii kwa urahisi.
Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo Jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miundombinu ya barabara iliyopo jimbo la ukonga katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Ndejembi ametoa wiki mbili kwa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha inakamilisha zoezi la usanifu wa barabara hiyo na kuwasilisha taarifa itakayoiwezesha Serikali kuiingiza kwenye mpango wa matengenezo kwa kiwango cha lami.
Ndejembi amesema kuwa, amelazimika kutoa maelekezo hayo kutokana na umuhimu wa barabara hiyo inayotegemewa na wananchi wa Pugu Stesheni katika kupata huduma za kijamii na kuongeza kuwa, barabara hiyo inaungana wakazi wa Mnadani, Kikuru na hivyo kuwa na manufaa kwa watumiaji wengi wa maeneo hayo.