Warusi Igor Girkin na Sergei Dubinsky na raia mmoja wa Ukraine Leonid Kharchenko ‘wamepatikana na hatia’ ya mauaji na kuhusika katika kuangusha ndege, Mrusi Oleg Poulatov ameachiliwa huru, jaji kiongozi Hendrik Steenhuis amesema. Watatu wa kwanza walipatikana na hatia bila kuwepo mahakamani, kwani wote wanne walikataa kuhudhuria kesi hiyo, iliyochukua miaka miwili na nusu.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwa upande wake amekaribisha “uamuzi huu muhimu”. “Adhabu kwa ukatili wote wa Urusi – jana na leo – haitaepukika,” ameongeza.
Ndugu wengi wa wahanga kutoka kote ulimwenguni walisafiri kwenda kusikiliza hukumu kwa kesi hii iliyotarajiwa sana katika mahakama yenye usalama karibu na uwanja wa ndege wa Amsterdam-Schiphol, ambapo Boeing 777 iliruka Julai 17 2014. Upande wa utetezi au wa mashitaka unaweza kukata rufaa.
Abiria na wafanyakazi wote 298 walipoteza maisha wakati ndege hiyo kutoka Amsterdam kwenda Kuala Lumpur ilipodunguliwa mashariki mwa Ukraine, eneo lililokuwa likishikiliwa na watu wanaounga mkono Urusi, na kile waendesha mashtaka wanasema ni kombora lililotolewa na Moscow. Majaji waliamua kwamba Igor Girkinen, Sergei Dubinsky na Leonid Kharchenko wote waliwajibika kwa kusafirisha kombora la BUK kutoka kambi ya kijeshi nchini Urusi na kulipeleka kwenye eneo la tukio, ingawa hawakuhusika peke yao. Hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuonyesha kwamba Oleg Pulatov, mshukiwa pekee aliwakilishwa na mwanasheria wake wakati wa kesi hiyo, alihusika, wamesema.