Kuelekea zoezi la uboreshaji wa Daftari la kudumu la mpiga kura, Makamu Mwenyekiti Tume huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC) Jaji Mstaafu Mbarouk Mbarouk amesema watu wenye mahitaji maalumu watapewa kipaumbele cha kujiandikisha bila ya kulazimika kusubiri kupanga foleni.
Ameyaeleza hayo leo wakati akifungua Mkutano wa Tume na Wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa uliopo Manispaa ya Iringa huku akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa haki za watu tajwa hapo juu zinaheshimiwa na kutekelezwa kwa usawa hivyo.
“Ni muhimu kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata fursa ya kushiriki katika uchaguzi bila kujali changamoto anazokutana nazo, Kwa hiyo watu wenye mahitaji maalumu watapewa kipaumbele maalumu katika vituo vya kujiandikisha ili wasiwekewe vikwazo vya aina yoyote na hakuna mtu atakayezuiliwa kutokana na hali yake ya kiafya au kimwili”, amesema Mbarouk.