Watuhumiwa watano wakiwemo raia wa China wawili, wanoakabiliwa na tuhuma za kuharibu Miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR) wamepandishwa kwa mara ya pili, katika mahakama ya Wilaya ya Kibaha, wakikabiliwa na makosa sita yakiwemo matano ya uhujumu wa miundombinu ya reli na utakatishaji wa fedha.
Akiwasomea mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Mhe. Felister Ngh’welo, mwendesha mashtaka wa Serikali Daudi Basaya, amesema watuhumiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo katika nyakati tofauti, kati ya mwezi Novemba na Desemba 2024 katika eneo la Miwaleni, Mlandizi Mkoa wa Pwani.
Mwendesha mashtaka huyo amewasomea mashtaka yao watuhumiwa, Wang Long Yu (62) raia wa China, Zang Dong Feng (55) pia Pius Kitulya (53) raia wa nchi jirani, Paul Joseph John (30) Mtanzania na Abduli Mohamed Mboya ambapo amesema katika nyakati tofauti walipatikana na mali zinazodhaniwa za wizi mali ya Shirika la Reli Tanzania, na kuitia hasara TRC ya shilingi zaidi ya milioni 217.