Watumishi wa Umma wanaotumia magari ya Serikali kwa matumizi binafsi watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ambapo Maafisa Masuuli wote wamekubushwa kusimamia maelekezo hayo.
Hayo yameelezwa leo Aprili 8,2024 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi Mha. Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mhe. Noah Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi aliyetaka kujua ni lini Serikali itazuia kupaki magari ya Serikali sehemu za starehe baada ya masaa ya kazi.
Mha. Kasekenya amesema Serikali kupitia Kanuni J.21 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 imezuia Watumishi wa Umma kutumia magari ya Serikali kwa matumizi binafsi, hivyo, mtumishi anayekwenda kinyume na maelekezo hayo anatakiwa kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu.
“Serikali kupitia Waraka wa Rais Na. 1 wa Mwaka 1998 kuhusu hatua za kubana matumizi ya Serikali, ilielekezwa kuwa magari yote ya Serikali yanatakiwa kuwa yameegeshwa sehemu zilizotengwa kwa ajili hiyo ifikapo saa 12.00 jioni bila kukosa vinginevyo kiwepo kibali rasmi kinachoruhusu gari la Serikali kuwepo barabarani baada saa 12.00 jioni,”amesema.