Watumishi watano kati ya sita wa Hospitali ya Wilaya ya Nansio Ukerewe wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa vyombo vya maadili ya utumishi wa umma pamoja na mabaraza na bodi za kitaaluma.
Watumishi hao tayari wamefikishwa Mahakamani kujibu tuhuma za wizi wa dawa zenye thamani zaidi ya Milioni 200 na mmoja wao alikiri na kuhukumiwa kulipa Milioni 100 na waliobaki walirejeshwa kazini.
Hata hivyo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Doroth Gwajima hivi karibuni aliagiza watumishi hao kusimamishwa kazi kufuatia Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Cornel Magembe kudai kuwa hakuridhishwa na watumishi hao kurejeshwa kazini kwani hawaaminiki tena kwenye utumishi wa umma na kamwe haiwezekani na haieleweki inawezekanaje mtumishi wa umma aibe halafu akishalipa anarejeshwa kazini.