Mkuu wa wilaya ya Iringa Komred Kheri James mapema leo amefanya kikao maalumu chenye lengo mahusisi la kutoa ujumbe kwa wazazi na walezi wa wilaya ya Iringa kuhusu malezi katika kipindi hiki ambacho Wanafunzi wameanza likizo.
Akizungumza katika kikao hicho Komred Kheri James ameeleza kuwa kutokana na ukweli kuwa jamii inakabiliwa na changamoto nyingi za vitendo vya ukatili, unyanyasaji na mmomonyoko mkubwa wa Maadili, Serikali imeona ni vyema kuzungumza na wazazi pamoja na walezi na kutoa ushauri maalumu ambao unaweza kusaidia kuwalinda watoto katika kipindi hiki cha likizo.
Komred Kheri James amewashauri wazazi wote wenye watoto wanaosoma madarasa ya mitihani kuwaruhusu kuendelea na ratiba zilizopangwa katika shule zao ili kuendelea kuandaliwa kikamilifu kuelekea katika mitihani yao ya kitaifa.
Aidha kwa Wanafunzi watakao kuwa nyumbani Komred Kheri James ameshauri wazazi kuwapangia ratiba za kujisomea wakiwa nyumbani, kuwapa fursa ya kujifunza stadi za maisha yaliopo nyumbani, kuwapeleka katika mafundisho ya dini, kufatilia mwenendo wa watoto, kutenga muda wa kutosha kukaa na watoto, kumpa nafasi mtoto kuonesha kipawa alicho nacho, Kumuunganisha na fursa zinazo inua uwezo wake wa kiakili na kimwili na kumjengea misingi ya kuishi vizuri na watu pamoja na kuzifahamu mila na desturi njema za jamii anayo ishi.
Komred Kheri James ameeleza kuwa ni wajibu wa kila mzazi kumlinda na kumjenga mtoto wake kuwa mtoto mwenye maadili mema ili aweze kuwa ni mtoto wa faida kwa familia na jamii kwa ujumla.
Pamoja na mambo mengine Komred Kheri James amesisitiza umuhimu wa jamii kuwalinda watoto dhidi ya ukatili, udumavu na hatari zote zinazo winda makuzi ya watoto.
Mheshimiwa Mkuu wa wilaya amewahakikishia wazazi kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kupambana na kuchukua hatua kali dhidi ya mtu yoyote atakae onekana ni kikwazo katika kuwalinda watoto na kusimamia maadili.
Kikao hicho maalumu cha wazazi kimehudhuriwa pia na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Viongozi wa Serikali, Wakuu washule, pamoja na Wazazi na Walezi.