Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, CP. Nicodemus Tenga, amewataka wazazi kutenga muda wa kuwa karibu na watoto wao, ili kuwapatia malezi bora na kuwaepusha na mmomonyoko wa maadili
CP. Tenga amesema kuwa wimbi kubwa la mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana na watoto linatokana na kulegea kwa mifumo ya malezi kuanzia ngazi ya wazazi wenyewe.
Akizungumza na wazazi na wahitimu wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Mzumbe, iliyopo mkoani Morogoro, Wilaya ya Mvomero, Kamishna Tenga alisisitiza kuwa ni muhimu kwa wazazi kuchukua hatua katika malezi ya watoto wao, ili kuwaepusha na vishawishi vinavyoweza kuathiri tabia zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa shule ya sekondari Mzumbe, Bw. Mbaraka Kupela, alielezea mafanikio ya kitaaluma ya shule hiyo, akisema kuwa shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya kujipima na mitihani ya kitaifa.
Hata hivyo, alizungumzia changamoto zinazokabili shule hiyo, zikiwemo miundombinu duni na uhaba wa vifaa vya kujifunzia, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha hali ya shule ili kuongeza ufaulu zaidi.
Aidha, akizungumza kwa niaba ya wazazi, mmoja wa wazazi aliwahimiza wahitimu kuhakikisha wanaepuka makundi yasiyo rasmi na kujitahidi kulinda heshima ya shule waliyomaliza. Aliwashauri wahitimu kuwa mfano bora kwa wengine, ili kuendeleza heshima ya shule ya sekondari Mzumbe.
Kamishna Tenga amemalizia hotuba yake na kusema kuwa wazazi wanapaswa kuwa na jukumu kubwa katika malezi ya watoto, kwa kuhakikisha wanapata elimu ya maadili na kujua umuhimu wa kuishi kwa heshima katika jamii. Alihimiza ushirikiano wa karibu kati ya wazazi na watoto ili kulinda maadili ya vijana.