NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvivu, Alexander Mnyeti, amemtaka Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Rukwa, Sultan Saleh Seif kuheshimu uamuzi wa Serikali wa kufunga shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kwa sababu kitendo chake cha kuwatangazia wananchi kuvua kwa kutumia ndoano ni sawa na kujifurahisha.
Kauli hiyo ya Serikali imekuja siku chache baada ya Seif kutumia mkutano wa hadhara uliofanyika tarehe 26 Juni mwaka huu katika Kijiji cha Ninde, Kata ya Ninde wilayani Nkasi mkoani humo, kuwatangazia wananchi kuwa wanaruhusiwa kuvua kwa ndoano pembezoni mwa ziwa hilo.
Serikali ilifunga shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kuanzia Mei 15 hadi Agosti 15 mwaka huu kwa lengo kupumzisha ziwa hilo ili kuwezesha samaki kuzaliana na kuongeza tija kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao ziwani humo.
Hata hivyo, MNEC huyo akitoa ufafanuzi zaidi kwenye chombo kimoja cha habari alidai akiwa katika mkutano huo wa hadhara alimpigia simu Mbunge wa jimbo hilo la Nkasi Kusini, Vincent Mbogo na kumueleza malalamiko ya wananchi kuhusu kuvua samaki wa mboga naye akamueleza kuwa wanaruhusiwa kuvua pembezoni mwa ziwa kwa kutumia ndoano na siyo wavu.
Hata hivyo, Mnyeti akizungumza na Mwandishi wetu jana tarehe 1 Julai, 2024 alisema inawezekana mbunge alipeleka ombi wizarani kuhusu wananchi wake kutumia ndoano na kukataliwa hivyo anatakiwa kuwa mvumilivu mpaka muda wa kufungua ziwa hilo tarehe 15 Agosti utakapofika.
Mnyeti alisisitiza kuwa Serikali haioni haja ya kubishana na MNEC Seif ambaye ndiye alisikika akiwatangazia wananchi hao kutumia ndoano kwenye ziwa hilo kwani utaratibu uliotangazwa na Serikali bado unaendelea kufuatwa hata na wananchi wanaoishi kwenye ukanda huo.
“Huyo MNEC sisi hatuna muda wa kubishana naye, kama alivyowatangazia wananchi tunamuona anajifurahisha tu kwa sababu wananchi wameheshimu maamuzi ya serikali kufunga shughuli za uvuvi kwenye ziwa hilo na matokeo wanayaona.
“Sasa inawezekana MNEC ameona kabisa samaki wameanza kuzaliana wapo pembezoni mwa Ziwa kutokana na matokeo ya uamuzi huu ndio maana akaamua kuwatangazia hivyo wananchi, ila niwaombe wananchi waisikilize serikali waendelee kuheshimu uamuzi tulioutoa kwamba hakuna shughuli za uvuvi wa aina yoyote hata ndoano, labda zinazoruhusiwa ni shughuli za usafiri tu,” alisema Mnyeti kwa msisitizo.
Itakumbukwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega alisema uamuzi wa Tanzania kufunga ziwa hilo unatokana makubaliano yaliyoazimiwa katika kikao kilichofanyika mwaka 2022 kikihusisha nchi zinazozunguka ziwa hilo ambazo ni Zambia, Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ulega alisema uamuzi huo ni utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika unaoweka hatua na taratibu za usimamizi endelevu wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.
Aliongeza uamuzi huo unatokana na utafiti uliobainisha kuwa kumekuwepo na upungufu mkubwa wa samaki na dagaa katika ziwa Tanganyika kunakotokana na ongezeko kubwa la uvuvi usio endelevu uliopelekea uharibifu wa mazalia ya samaki.