Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amekutana na wananchi wa Engaruka katika zoezi la uhamasishaji kuelekea ulipaji wa fidia kwa wakazi wa maeneo ambapo serikali inatarajia kulipa kiasi cha shilingi bilioni 14.4 kwa wananchi wanaotarajia kupisha utekelezaji wa mradi wa maendeleo wa Engaruka, Monduli-Arusha.
Akizungumza mbele ya viongozi wa Serikali, wananchi, na waandishi wa habari, Dkt. Jafo alisisitiza dhamira ya Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha fidia inalipwa kwa uwazi, haki, na kwa kuzingatia thamani halisi ya mali za wananchi.
Waziri alisisitiza kuwa Serikali imehakikisha kuwa jumla ya wafidiwa 595 watalipwa fidia kwa kiwango kinacholingana na tathmini iliyofanyika. Alieleza kuwa hakuna mwananchi atakayedhulumiwa au kupunjwa malipo.
Ili kuhakikisha matumizi bora ya fedha za fidia, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na taasisi nyingine za kifedha kama UTT-AMIS, NEEC, NMB, na CRDB, imeandaa semina za kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya fedha hizo. Waziri aliwasihi wanufaika wote kushiriki katika semina hizo.
Waziri alieleza kuwa mradi wa uchimbaji wa madini ya Magadi Soda unaotarajiwa kuanza mara baada ya ulipaji fidia, utatoa ajira kwa wananchi wa eneo husika na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Dkt. Jafo alihitimisha kwa kuwataka wananchi wa Engaruka kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa bila changamoto.
“Serikali iko nanyi, na dhamira yetu ni kuona kila mmoja wenu anapata haki yake. Tushirikiane kuhakikisha mafanikio ya pamoja,” alisisitiza