Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Yusuf Makamba (Mb) amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Vatican nchini, Mhe. Angelo Accattino yaliyofanyika Aprili 02, 2024 katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine, yalilenga kujadili hatua za utekelezaji wa masuala yaliyokubaliwa wakati wa ziara ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika
Vatican tarehe 11 na 12 Februari 2024 kufuatia mwaliko wa Papa Francis II, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani.
Aidha, wawili hao walisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Vatican katika masuala ambayo pande mbili zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu. Masuala hayo ni pamoja na utoaji wa huduma za kijamii kama vile elimu na afya, mchango wa Vatican na Taasisi za kidini katik kuhamasisha amani na mshikamano nchini.
Mhe. Accattino aliisifu Tanzania kwa kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika kutokana na mchango wake wa muda mrefu katika kuhamasisha amani na usalama barani Afrika na kuahidi kuwa Vatican itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala mbalimbali muhimu kwa ustawi wa Taifa.
Kwa upande wake, Mhe. Makamba alielezea furaha yake kufutia ziara yenye mafanikio makubwa aliyoifanya Mhe. Rais huko Vatican na kueleza kuwa Tanzania itatekeleza masuala yote yaliyokubaliwa wakati wa ziara hiyo.