Ikiwa ni Jitihada za Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki ya kiuwekezaji katika Sekta ya Madini nchini, Wizara ya Madini na Chemba ya Migodi zimekutana Oktoba 27, 2023, ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu uliowekwa na Wizara kukutana na Wachimbaji Wakubwa, wa Kati na Watoa huduma migodini kila Robo ya Mwaka kupitia Chemba ya Migodi.
Mkutano huo ni wa Pili kufanyika baada ya mkutano wa kwanza uliofanyika mapema mwezi Julai, 2023, yote ikilenga kuleta ukaribu kati ya serikali na wadau wa sekta ya madini pamoja na kujadili kwa pamoja changamoto ili kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyozuia utekelezaji wa miradi, shughuli na biashara ya madini nchini.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ambaye amekutana na wadau hao kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa na kuapishwa kuwa Waziri wa Madini, amesema, mikutano hiyo inatumika kama njia ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa miradi wanayoisimamia ili kuchochea uwekezaji.
‘’Tukiondoa vikwazo itasaidia kuongeza shughuli za uchimbaji nchini na hatimaye tutaongeza uchumi na mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa, tutaongeza ajira, maendeleo ya nchi na watu. Chukulia mfano wa Mkoa wa Geita tu, Serikali inakusanya shilingi bilioni 243, tunataka shughuli za madini zifanyike mikoa yote katika mazingira rafiki,’’ amesisitiza Mavunde.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde amefungua mlango kwa wawekezaji wote nchini na kueleza kuwa hategemei kuwa kikwazo kwao na kuwataka kuendelea kushirikiana na Serikali kuendeleza Sekta ya Madini nchini.