Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hali ya uzito uliozidi na uzito uliokithiri (kiribatumbo) ndicho kiashiria pekee ambacho hakijawahi kupungua na kimeendelea kuongezeka kutoka asilimia 11.3 mwaka 1991 hadi kufikia asilimia 31.7 mwaka 2018 kwa Tanzania Bara na kwa Zanzibar uzito uliozidi umefikia asilimia 41.8 katika kipindi hichohicho.
Amesema tatizo la uzito uliozidi na kiribatumbo ni kubwa katika Mikoa ya Kilimanjaro ambako wana asilimia 49, Dar es Salaam (asilimia 48.6), Mjini Magharibi (asilimia 47.4) na Kusini Unguja (asilimia 39.4).
Amesema hayo leo Jumamosi, Aprili Mosi, 2023 wakati akizungumza na Maelfu ya Wakazi wa Mtwara na Mikoa ya jirani waliofika kushuhudia uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Nangwanda Sijaona, katika Manispaa ya Mtwara.
“Hali hii inaelekea kuwa janga la kitaifa na kisababishi kikubwa cha kuongezeka baadhi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, saratani na magonjwa ya moyo, Wananchi wenzangu, sasa ni wakati muafaka wa kubadili mitindo ya maisha yetu kwa kufanya mazoezi angalau nusu saa kila siku na kula mlo kamili sambamba na kuepuka vyakula vyenye mafuta mengi, sukari nyingi, pombe na sigara”